Ngano na Elimu ya Kimagharibi: Mustakabali wa Ngano za Kinyankole katika Karne ya 21
Abstract
Makala hii inatokana na utafiti ambao tulifanya katika jamii ya Wanyankole kuhusu usimulizi wa ngano za Kinyankole kwa mikabala ya kiutendoneni na kiuamilifu. Katika utafiti huu, iligunduliwa kwamba ngano za Wanyankole zinaelekea kudidimia na kutoweka kabisa na wanalaumu elimu ya Kimagharibi. Kulingana na Wanyankole walioshuhudia jinsi mambo yalitendeka miaka kama sabini na zaidi iliyopita, usimulizi wa ngano ulikuwa nyenzo na fursa ya wanajamii kutagusana na kukuza hisia ya umoja na utambulisho wa kijamii. Ngano zao zilikuwa na majukumu mahsusi ambayo zilitekeleza katika harakati za kujamiisha wanajamii. Pamoja na hayo, ziliburudisha wanajamii papo hapo. Licha ya majukumu ambayo ngano hizi zilitekeleza na burudani ambayo zilitoa, zinaelekea kudidimia kwani, hazisimuliwi tena kama ilivyofanywa enzi za jadi. Je, ni kweli kwamba kudidimia kwa ngano zao kumesababishwa na elimu ya Kimagharibi? Ni kwa kiasi gani elimu hii imechangia kudidimia kwa ngano za Kinyankole? Wanyankole ambao mtafiti alikutana nao walionekana kupoteza matumaini wakilalamika kuwa usimulizi wa ngano zao huenda hautarudi kwa sababu mfumo wa elimu iliyopo hauna nafasi ya kuendeleza ngano zao. Je, kuna namna elimu inaweza kutumiwa kuendeleza ngano za Kinyankole? Haya ni baadhi ya maswali ambayo makala hii ilitazamia kujibu. Makala hii iliongozwa na nadharia ya uamilifu kama iliyoendelezwa na Malnowisk (1922) na kuboreshwa baadaye na Mesthrie na wenzake (2004). Makala hii imehitimisha kwamba elimu ya Kimagharibi imechangia kudidimia kwa ngano za Kinyankole. Matokeo ya makala hii yamechangia maarifa kuhusu jinsi elimu ya Kimagharibi inaweza kutumiwa kuhifadhi na kuendeleza ngano za Wanyankole.
Istilahi Muhimu: Wanyankole, Kinyankole, Elimu ya Kimagharibi, Kudidimia